Nehemiah 9:25-30

25 aWakateka miji yenye ngome na nchi yenye rutuba, wakamiliki nyumba zilizojazwa na vitu vizuri vya kila aina, visima vilivyochimbwa tayari, mashamba ya mizabibu, mashamba ya mizeituni na miti yenye matunda kwa wingi. Wakala, wakashiba nao wakanawiri sana, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.

26 b“Lakini hawakukutii nao wakaasi dhidi yako, wakatupa sheria zako nyuma yao. Wakawaua manabii wako, waliowaonya ili wakurudie, na wakafanya makufuru makubwa. 27 cHivyo ukawatia mikononi mwa adui zao, ambao waliwatesa. Lakini walipoteswa, wakakulilia wewe. Kutoka mbinguni uliwasikia, nawe kwa huruma zako kuu ukawapa waokozi, waliowaokoa kutoka mikononi mwa adui zao.

28 d“Lakini mara walipokuwa na raha, wakafanya maovu tena machoni pako. Kisha ukawaacha mikononi mwa adui zao, nao wakawatawala. Walipokulilia tena, ukasikia kutoka mbinguni, na kwa huruma zako ukawaokoa kila mara.

29 e“Ukawaonya warudi katika sheria yako, lakini wakawa na kiburi na hawakutii amri zako. Wakatenda dhambi dhidi ya maagizo yako ambayo kwayo mtu ataishi kama akiyatii. Kwa ukaidi wakakugeuzia kisogo, wakawa na shingo ngumu na wakakataa kusikiliza. 30 fKwa miaka mingi ulikuwa mvumilivu kwao. Kwa njia ya Roho wako ukawaonya kupitia manabii wako. Hata hivyo hawakujali, basi ukawatia mikononi mwa mataifa jirani.
Copyright information for SwhKC